Masaibu ya Kushabikia Stars

March 29, 2016 By Fabian Odhiambo

Masaibu ya Kushabikia Stars

Kwanza kabisa, ningependa kuwaomba radhi enyi wasomaji wetu tunaowaenzi na kuwathamini si haba. Kwa kawaida mitungo yote kwenye The Dug Out huwa imeandikwa kwa lugha ya Kimombo, lakini kwa vile leo twagusia masaibu ya timu yetu ya taifa, tutajaribu kuswahilisha hisia zetu, angalau kwa leo tu, pia ndiposa ujumbe upate kuwafikia wengi wa wananchi wenzetu.

Naam, pengine tuseme makiwa? Kwa mara nyingine timu yetu ya Harambee Stars imeshindwa kufuzu kwenye dimba lolote lile la kimataifa, hususan kinyang’anyiro cha Bara la Afrika kitakachosakatwa mwaka ujao huko Gabon. Hii ni kufuatia kupoteza mechi mbili muhimu kwa muda wa siku nne mikononi mwa Guinea Bissau, ugenini na nyumbani. Michwano hiyo miwili kwa kweli ilikuwa ya kimsingi ikiwa tulikuwa tufufue matumaini yetu ya kukata tikiti ya kwenda Gabon. Kupata matokeo mazuri kwenye hizo dakika mia moja themanini ilikuwa lazima kama ibada, lakini dau la mnyonge haliendi joshi, na sisi hao, wanyonge wa kandanda barani.

Swali ni, je, ni hadi lini tutakuwa wanyonge? Rais wa shirikisho la mchezo wa kabumbu nchini, Bwana Nick Mwendwa inasemekana keshanong’onezea taifa kwa jumla ya kwamba yale mabadiliko tuliyoyatarajia kwa hamu na ghamu kamwe hatutayaona hadi manmo mwaka wa 2019, yaani miaka mitatu ijayo. Salale! Mbona tena iwe hivo? Mataifa mengine yatakuwa yakiona mchezo wao ukiwanda na kunawiri ilhali sisi tukibaki nyuma mithili ya koti kwa hiyo miaka mitatu tumaini letu kuu likiwa ni ule msemo wa jadi kuwa Mungu hamkoseshi mja wake? Hata ikiwa hivo jameni, si ni bayana kwamba huyo Rabuka mwenyewe husaidia tu wale wanaojisaidia?

Nick Mwendwa ni kama amesahau ya kwamba wakati wa kampeni umekwishapita kitambo, na sasa si wakati wa ahadi, bali wa kazi. Yuafaa ajue kuwa ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo. Utapewaje jembe uende ukalime leo nawe ukadai ni pengine katika wiki zijazo ndo mikono yako itakukubalia kushika hilo jembe? Hatuwezi, kama wapenzi wa soka humu nchini kukaa tu mbumbumbu kwa sababu Mwendwa ameonelea ni haki tungoje. Yeye yuataka kaa, basi na sisi tutampa moto!

Mengi yamesemwa kuhusu uteuzi wa Stanley Okumbi kama mkufunzi wa timu ya taifa. Hata sisi hatukuachwa nyuma kwenye hoja hilo, hapa. Ukweli ni kwamba wengi wetu hawajaridhishwa na jambo hilo, lakini yamemwagika, hayazoleki. Ni yeye aliyetwaa usukani kwa wakati huu kwa hivyo hatuna budi kuitikia wito wa rais wa shirikisho wa kumpa nafasi ya kutenda kazi.

Kuna mambo machache hapa na pale ambayo Okumbi anapswa kujua na kutilia manani. Ni jukumu lake kuchagua kikosi bora kila tukiwa na mechi ya aina yoyote ile. Wiki jana katika mkondo wa ugenini huko Bissau, utata ulizuka kuhusu wachezaji fulani waliotajwa kufuatia uzoefu na pia uhodari wao hususan kiungo cha kati, Pattilah Omotto. Naam, wakenya wenza, hatuna ugomvi au vita naye Omotto na sisi sote twamtakia kila la heri katika usakataji wake wa kandanda. Mwendwa akitetea amuzi hilo alisema ya kwamba wachezaji barobaro lazima wapewe fursa ili wao pia wapate uzoefu wa kucheza katika jukwaa la kimataifa. Na ni wazo la busara, hilo. Lakini twasema hivi: chagua, kati ya hao vijana wote, wale ambao ujuzi wao hauna tashwishi hata chembe. Pia kwa kawaida katika nchi nyingine, kikosi kikitajwa, wale wachezaji wachanga hujumuishwa lakini kwa madhumuni tu ya kujitia makali na wale wenye uzoefu ili kuwatayarisha kwa siku za usoni zamu yao itakapowadia. Haifai kuwarusha kwenye dimbwi la kuanza katika mechi muhimu – huenda wakazama mapema ikawawia vigumu hata kujaribu kuogelea baadaye.

Neno ‘maandalizi’ katika sekta hii ya kandanda limekuwa tu ni neno tunaoweza kulipata kwenye kamusi. Hakuna jambo lolote lile ambalo laweza kufanikishwa bila maandalizi. Na sio tu maandalizi, bali maandalizi kabambe. Ni lini ulisikia ya kuwa Harambee Stars iliandaa mechi ya kirafiki na taifa jingine ili kujipima nguvu? Usijali, nitangoja jibu lako. Na sisemi mechi dhidi ya vilabu vya ligi kuu ya Kenya kama Posta Rangers na kadhalika. Hebu fikiria, waenda kuchuana na mataifa mengine ambayo pia yana matumaini ya kufuzu kwenye dimba la Kombe la Dunia ama Bara la Afrika halafu wajipima nguvu na timu finyu kama hizo la ligi. Haisaidii kamwe! Wazee husema utavuna ulichokipanda, na hawatuhadai. Ni sharti sisi pia tuige mfano wa mataifa mengine na kuanza kuandaa mechi za kirafiki yenye manufaa dhidi ya hayo mataifa.

Kwa wakati huu kama taifa la Kenya linaloshabikia vilivyo mchezo wa kandanda tumezama kwenye majonzi isiyo na kifani. Biwi la simanzi limetanda viwanjani na nyumbani mwetu kuhusiana na hatima ya harakati zetu za kufika Gabon mwaka ujao. Lakini penye nia pana njia, ndiposa twasema ni wakati wa kuungana pamoja na kutoa maarifa yetu ili kuimarisha hali ya mchezo wetu. Hakuna marefu yasiyo na ncha.

Kama ilivyo itikadi, hakikisha umetupigia kura kwenye kitengo cha Blogu bora ya Spoti hapa. Shukran!

%d bloggers like this: