Utata wa Kushabiki

March 7, 2015 By Fabian Odhiambo

Utata wa Kushabiki

Je, wewe ni shabiki wa aina gani? Ama, wafaa kuwa shabiki wa aina gani? Ni swala ambalo limenitatiza si haba. Kwa kila mpenzi wa mchezo wa kabumbu, au mchezo wowote ule ni lazima kama ibada kuiunga mkono timu yako kwa vyovyote vile, kwa udi na uvumba. Ila, kuna jambo. Je, hakuna nafasi ya kukashifu matokeo ama utendaji kazi wa timu kwa madhumuni ya kuwepo kwa marekebisho?

Majuzi nimejipata matatani katika kikundi chetu cha wapenzi wa soka. Swala lilikuwa ni, je, kwa maoni yako, wadhani kuna uwezekano wa Arsenal kuitimua Manchester United kutoka kwa dimba la FA wakutanapo kwenye robo fainali siku ya Jumatatu tarehe tisa Machi mwaka huu? Basi, kwa kawaida mimi ni wa Arsenal lakini kwa hilo swali, hata uniamshe usiku wa manane kutoka kwa usingizi wa pono, jibu langu litakuwa ‘la hasha!’ Kuipigia debe vijana wa Arsene Wenger katika mchuano huo ni kama kupanda mgomba kwenye changarawe – haupandwi ukamea. Isitoshe, mechi hiyo itachezwa ugani Old Trafford. Itakumbukwa kwamba tangu mwaka wa 2006, Arsenal haijailaza United ugenini. Si utakubaliana nami kwamba kutokana na ushaidi huo, sikuwa nimekosa sana kwa kutoa hukumu kali kwa timu hiyo niipendayo?

Shutuma iliyoelekezwa kwangu ni kuwa mimi si shabiki halisi. Eti shabiki halisi yuafaa kuamini ya kwamba timu yake itashinda mechi ijaayo, liwe liwalo hata kama ni dhahiri shahiri kuwa harakati zao zaelekea kugonga mwamba. Haiya! Maajabu hayo. Miye Mgalla, mniuwe, lakini haki mnipe, wenzangu. Nikitabiri kwamba timu ninayoishabikia itagaragazwa na mahasimu wao wa jadi walio na mazoea ya kuwafedhehesha miaka nenda miaka rudi, itakuwaje naathiri hali ya mchezo wa wachezaji wetu? Kivipi? Si mmoja wenu asimame kidete aniambie?

Kamwe sitoshikilia maoni hayo kwamba chochote tusemacho sisi wanaotizama mpira chaathiri anayesakata kandanda upande ule mwingine wa dunia. Sidhani vinywa vyetu vishapewa kipawa kama hicho. Hao wachezaji wa Arsenal kwangu mimi kuku ni kama mwewe na tangu lini dua la kuku likampata mwewe?

Hakuna mja yeyote ambaye anaweza akatakia timu yake mabaya. Na kama kunaye, hebu ajitokeze hadharani umati umjue na kumkashifu. Kila mwamba ngozi huivuta kwake (kwa timu yake). Kuna wale ambao hawaoni doa kwa waipendayo na pia ni sawa tu. Halafu kunao wengine wetu waliojizamisha kwenye bahari ya uhalisia, walio tayari kusema yale ambayo hayatakubaliwa na wengi. Kuna makosa gani hayo? Si kila mzimu na shetani wake?

Kwa tamati, hiyo mechi ya usiku wa Juamatatu itakuwa ngumu. Licha ya kwamba nahofia mabaya, natumai dau litaenda joshi bila bughudha nyingi. Mimi ni zimwi nijuaye Arsenal, siwezi nikaila nikaimaliza.

%d bloggers like this: